BAADHI YA SALA NYINGINE (#11223)

Utukufu uwe Kwako Ee Mungu, kwa ajili ya Ufunuo wa Pendo lako kwa wanadamu!  Ee Ewe Uliye Uzima na Mwanga wetu, ongoza watumishi Wako katika njia Yako, ututajirishe ndani Yako na kuwa huru kwa yote ila Wewe tu. 

Ee Mungu, utufundishe umoja Wako na utupe utambuzi wa Umoja Wako ili tusione yeyote ila Wewe.  Wewe u Mwenye Rehema na Mpaji wa Ukarimu! 

Ee Mungu, washa katika mioyo ya wapendwa Wako moto wa upendo Wako ili uteketeze mawazo ya kila kitu ila Wewe. 

Tufunulie, Ee Mungu, milele Yako iliyotukuka – kwamba Wewe umekuwako, na utakuwako, na kwamba hakuna Mungu mwingine ila Wewe tu.  Hakika faraja na nguvu vinapatikana kwako.

-Bahá'u'lláh
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11224)

Ee Mungu wangu!  Ee Mungu wangu!  Unganisha mioyo ya watumishi Wako na uwafunulie kusudi Lako lililo kuu.  Wafuate amri Zako na kukaa katika sheria Yako Uwasaidie, Ee Mungu katika jitihada yao, na uwape nguvu kukutumikia.  Ee Mungu, usiwaache peke yao bali uongoze hatua zao kwa mwanga wa maarifa yako na furahisha mioyo yao kwa upendo Wako. Hakika, Wewe ndiwe Msaidizi na Bwana Wao.

-Bahá'u'lláh
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11225)

Sema:  Ee Mungu, Mungu wangu!  Vika kichwa changu kwa taji la haki na paji la uso wangu kwa pambo la uadilifu.  Wewe, hakika, u Mwenye vipaji na baraka zote.

-Bahá'u'lláh
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11226)

Ee, Mungu wangu!  Nakuomba kwa Jina Lako tukufu kabisa, kunisaidia katika lile litakalofanya shughuli za watumishi Wako kufanikiwa, na miji Yako kusitawi.  Wewe, kweli, una uwezo juu ya vitu vyote!

-Bahá'u'lláh
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11227)

Mungu jalia kwamba nuru ya umoja iweze kufunika dunia yote, na kwamba mhuri, “Ufalme ni wa Mungu” uweze kupigwa juu ya paji la uso la watu wake wote.

-Bahá'u'lláh
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11228)

Kuna mwondoa shida yeyote isipokuwa Mungu?  Sema: Mungu asifiwe!  Yeye ni Mungu!  Wote ni watumishi Wake, na wote wanaishi kwa mapenzi Yake!

-The Báb
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11229)

Ee Mungu, changamsha na uifurahishe roho yangu.  Takasa moyo wangu.  Ng’arisha fikira zangu. Naacha shughuli zangu zote mikononi Mwako.   Wewe U kiongozi na kimbilio langu..  Sitakuwa na majuto wala kuhuzunika tena, nitafurahi na kuchangamka.  Ee Mungu!  Sitajawa na mashaka tena, wala sitaacha taabu zinisumbue tena.  Sitaishi kwa vitu visivyofaa maishani. 

Ee Mungu! Wewe U rafiki kwangu zaidi ya mimi nilivyo mweneyewe kwangu. Najitoa mwenyewe Kwako, Ee Bwana.

-`Abdu'l-Bahá
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11230)

Ee Bwana wangu, Mpendwa wangu, Haja yangu!  Nifanye rafiki katika ukiwa wangu na ufuatane nami katika uhamisho wangu.  Ondoa huzuni yangu.  Nifanye kujitoa kwa uzuri Wako.  Nitoe kwa vyote ila Wewe.  Nivutie kupitia manukato Yako ya utakatifu.  Nifanye kuwa mshirika katika Ufalme Wako na wale ambao wamejitenga na yote isipokuwa Wewe na wanaotamani kuhudumu katika enzi yako takatifu na wanaosimama kufanya kazi katika Hoja Yako.  Uniwezeshe kuwa mmoja wa watumishi wako wa kike ambao wamepata ridhaa Yako njema.  Hakika, Wewe ni mwenye Rehema, Karimu.

-`Abdu'l-Bahá
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11231)

Ee Bwana Mungu wangu!  Wasaidie wapendwa Wako kuwa imara katika Imani Yako, kutembea katika njia Zako, kuwa dhabiti katika Hoja Yako.  Wape neema Yako kuzuia mashambulio ya nafsi na tamaa, kufuata mwanga wa Uongozi Mtakatifu.  Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye rehema, Aishiye Mwenyewe, Mpaji, Mwenye huruma, Mwenyezi, Karibu) kabisa.

-`Abdu'l-Bahá
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11232)

Bwana, sisi tu watu wa kuhurumiwa, utupe kibali Chako; tu maskini, utupe fungu kutoka kwa wingi wa ukwasi Wako; tu wenye haja, ututosheleze; tumetahayarishwa, utupe neema Yako.  Ndege wa anga na wanyama wa konde wapokea chakula chao kutoka Kwako kila siku na viumbe wote wana ulinzi na upendo Wako. 

Usimnyime mnyonge huyu neema Yako ya ajabu na uijalie nafsi hii dhaifu Baraka Yako kwa nguvu zako. 

Utupe hakula chetu cha kila siku na utuongezee maisha yetu, ili tusitegemee yeyote ila Wewe, tuzungumze nawe, tutembee katika njia Zako na kutangaza mafumbo Yako.  Wewe u Mwenyezi na Mwenye upendo na Mpaji wa wanadamu.

-`Abdu'l-Bahá
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11233)

Ee Bwana!  Sisi tu wanyonge; tuimarishe.  Ee Mungu! Tu wajinga; tufanye wajuzi.  Ee Bwana!  Tu maskini; tufanye matajiri.  Ee Mungu!  Tu wafu; tuhuishe.  Ee Bwana!  Sisi tu fedheha yenyewe; tutukuze katika Ufalme Wako.  Ukitusaidia, Ee Bwana, tutakuwa kama nyota zimemetekazo.  Usipotusaidia, tutakuwa na hali ya chini kuliko udongo. Ee Bwana!  Tuimarishe.  Ee Mungu!  Tujalie ushindi.  Ee Mungu! Tuwezeshe kushinda nafsi na tamaa  Ee Bwana!  Tuokoe kutoka katika utumwa wa mambo ya kidunia.  Ee Bwana!  Tuhuishe kupitia pumzi ya Roho Mtakatifu ili tuamke kukutumikia, tujishughulishe katika kukuabudu Wewe na kujibidiisha wenyewe katika ufalme Wako kwa ukweli kabisa.  Ee Bwana!  U Mwenye nguvu!  Ee Mungu, U Msamehevu!  Ee Bwana, U Mwenye Rehema!

-`Abdu'l-Bahá
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11234)

Ee Mungu, Mungu wangu!  Wakinge watumishi Wako waaminifu na maovu ya tamaa walinde na jicho Lako la upendo dhidi ya chuki, karaha ni kijicho, uwahifadhi katika Neno Lako lisilopotoka wawe salama kwa mishale ya mashaka, wafanye wajumbe wa ishara Zako tukufu, ng’arisha nyuso zao kwa miale inayong’aa itokayo katika chimbuko la umoja Wako mtukufu, furahisha mioyo yao kwa maneno yatokayo katika ufalme Wako mtukufu na tia nguvu viuno vyao kwa nguvu itokayo katika milki Yako tukufu.  Wewe ni Mwenye Baraka Zote Mlinzi, Mwenyezi na Mwenye rehema.

-`Abdu'l-Bahá
-----------------------

BAADHI YA SALA NYINGINE (#11235)

Ewe Mungu!  Ewe Mungu!  Huyu ni ndege aliyevunjika mabawa yake na kuruka kwake ni shida sana.  Msaidie ili kwamba aweze kuruka kwa upeo wa ufanisi na wokovu, wekelea kuruka kwake kwa furaha kuu na upendo katika nafasi isiyo na kikomo, inua sauti yake katika Jina Lako tukufu ndani ya sehemu zote, changamsha masikio na mwito huu, na ng’arisha macho kwa kutazama dalili za maongozi! 

Ewe Bwana!  Mimi ni pweke, mmoja na aliye chini.  Kwangu mimi sina wa kutegemea ila Wewe, sina wa kunisaidia isipokuwa Wewe na sina wa kunihifadhi kando Yako.  Nithibitishe katika kazi yangu, nisaidie na majeshi ya malaika Wako, nifanye mshindi katika kuendeleza neno Lako na uniwezeshe kunena kutoka kwa hekima Yako juu ya viumbe Wako.  Hakika Wewe U Mtunza maskini na Mtetezi wa walio wadogo na kweli U Mwenye nguvu, Mwenye uwezo na Asiyeshurutishwa!

-`Abdu'l-Bahá
-----------------------

